Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Kwa muda mrefu kumekuwa na dhana kuwa wazee ndiyo wanaoposwa kuwa matajiri kwa kuwa wamefanya biashara kwa muda mrefu na kupata faida kubwa. Hata hivyo, kibao kimeanza kugeuka baada ya kuanza kuibuka kwa mamilionea wenye umri mdogo.
Miongoni mwa vijana hao wapo barani Afrika. Katika orodha hiyo Tanzania haikuachwa mbali, kwani kwa mujibu wa Jarida la Forbes linalochambua masuala ya utajiri na matajiri, wafanyabiashara Ally Edha Awadh na Mohammed Dewji ni miongoni mwa mamilionea hao.
Awadhi ni msambazaji na msafirishaji wa nishati na mafuta, pia ni Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya Lake Oil Group, ikiwa ni moja ya kampuni ya inayokuwa haraka Afrika Mashariki. Awadhi anasema kuwa kampuni hiyo aliianzisha mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 23.
Anasema mafanikio yake yalianza kuonekana baada wa Serikali ya Tanzania kumpa kibali cha kuingiza mafuta na bidhaa mbalimbali zinazohusiana na mafuta nchini.
Hivi sasa Lake oil ni moja ya kampuni tano kubwa zinazosambaza mafuta nchini na katika nchi za jirani za DR Congo, Zambia, Burundi and Rwanda. Pia kampuni hiyo ina tangi kubwa la kuhifadhia mafuta katika eneo la Kigamboni lenye ujazo wa lita 35, 000,000.
Pia Kampuni ya Lake Trans ya Awadhi inamilika tabribani malori 500 yanayofanya safari zake ndani na nje ya nchi.
Mohammed Dewji (39) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Ltd (METL Group), moja ya kampuni kubwa Afrika Mashariki. Dewji ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mjini, anatajwa kufanikiwa kuendeleza kwa mafanikio biashara iliyokuwa imeanzishwa na baba yake, Gulam Dewji zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Dewji amefanikiwa chini ya kampuni yake kuzalisha nguo, sabuni, mafuta, baiskeli na vinywaji. Kampuni hiyo kwa mwaka inapata zaidi ya dola 1.5 bilioni ikiwa na zaidi ya wafanyakazi 24,000.
Kwa mujibu wa Forbes, Dewji anashikilia nafasi ya 38 kwa utajiri Afrika. Katika kuhakikisha kuwa anatoa mchango wake kwenye uboreshaji wa elimu, huduma za afya na umasikini, Dewji au Mo kama anavyofahamika na wengi, ameanzisha taasisi ijulikanayo kama Mo Dewji Foundation.
Katika orodha hiyo yupo pia mfanyabiashara kutoka Nigeria, Alexander Amous, (38) anayesifika kwa kubuni bidhaa za gharama kubwa, yakiwamo makava ya simu yenye almasi na vifaa vingine.
Amosu alianza kuingiza fedha wakati akiwa na umri wa miaka 24 alipoanza kuuza milio kwenye kampuni za simu nchini Uingereza. Kutokana na mafanikio hayo alianzisha kampuni ya kutengeneza milio ya R&B. Kampuni hiyo ilimpatia faida ya dola 1.5 milioni katika mwaka wa kwanza wa utendeji wake. Hata hivyo, Amosu aliiuza kampuni hiyo mwaka 2001 kwa dola 15milioni.
Kampuni yake nyingine ya Kamson Luxury Group inajishugulisha na uchajishiaji wa jarida la OK, linalozungmza watu maarufu nchini.
Kijana mwingine milionea ni Sim Shagaya (38) kutoka Nigeria. Mfanyabiashara huyo ni msomi wa shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Harvard. Ni mwanzilishi wa kampuni kubwa kufanya biashara kwa njia ya mtandao ya Konga.com.
Kampuni hiyo iliyoanzisha Julai 2012, imekwishaingiza zaidi ya dola38 milioni kutoka kwa wawekezaji wengine kama Kinnevik na kampuni kubwa ya habari ya Afrika Kusini, Naspers. Pia milionea huyo ni mwanzilikishi wa kampuni nyingine ya site na E-Motion, inayojishughulisha na matangazo.
Kijana mwingine aliiyeingia kundi la watu mamilionea ni Dennis Makori (34) kutoka Kenya, ambaye kampuni yake ya Onfon Media inaingia kiasi kikubwa cha fedha kwa kutoa huduma za simu na takwimu. Kampuni hiyo ina wafanyakazi zaidi ya 60 katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda na Ghana. Kwa mwaka inakusanya jumla ya Dola3 milioni.
Mwingine ni Adii Pienaar (29) kutoka Afrika Kusini, ambaye Kampuni yake ya Woothemes, inayojishughulisha na ubunifu wa matangazo kwenye mtandao wa WordPress. Kampuni hiyo ilianzishwa 2007 kwa bajeti ndogo iliyokuwainaiwezesha kupata dola3 milioni kwa mwaka.
Kijana huyo pia ni mwanzilishi wa Kampuni ya Public Beta, ambayo inawawezesha wajasiliamali wakubwa kutoa ujuzi kwa wengine wanaotaka kuingia katika fani hiyo.
Huko huko Afrika Kusini, yupo kijana Colin Thornton (34), mwanzilishi wa Kampuni ya Dial-A-Nerd inayotoa huduma za komputa nyumbani na maofisini. Thornton alianzisha kampuni hiyo baada ya kuacha masomo katika Chuo Kikuu cha Witwatwesrand alikokuwa akisomea sayansi ya kompyuta.
Kwa mwaka kampuni hiyo inaingiza zaidi ya dola10 milioni, ikiwa na matawi 14 Afrika Kusini na wafanyakazi 150.
Mike Macharia (36), kutoka Kenya ndiye mmiliki wa Kampuni ya Seven Seas technology, iliyoanzishwa miaka 10 iliyopita, ikitoa huduma za kiteknolojia na mawasiliano. Kampuni hiyo kwa mwaka inapata zaidi ya dola50 milioni pia ipo katika mkakati wa kusajiliwa kwenye soko la hisa la Nairobi.
Pia, Ken Njoroge (38) naye wa Kenya ametajwa kuingia katika kundi la vijana milionea Afrika baada ya Kampuni yaCellulant aliyoianzisha kwa ushirikiano na rafiki yake kutoka Nigeria, Goke Akinboro kwa mtaji wa dola120 milioni.
Kampuni hiyo inajishughulisha na utoaji huduma za kusambaza nyaraka na stakabadhi ya njia ya mtandao wa simu ikiwa na matawi katika nchi nane za Afrika.
Bethlehem Tilahun Alemu (34) kutoka Ethiopia ameingia kwenye orodha ya mamilionea wa Afrika baada ya kampuni yake ya kutengeneza viatu ya SoleRebels kufanya vizuri sokoni. Mpaka sasa kampuni hiyo ina utajiri wa dola tano milioni kwa mwaka.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment