Wednesday, 21 January 2015

Panya Road

Panya Road katika jicho la Tehama

Ilikuwa jioni muda wa saa tisa hadi kumi baadhi ya watu walioko katikati ya jiji la dar es salaam walipokea ujumbe mfupi kwenye simu zao kwamba kundi la Panya Road limeteka baadhi ya mitaa na wanatishia watu.
Nao waliopata ujumbe kwa njia ya simu walianza kuweka kwenye mitandao ya mawasiliano hasa ya kijamii. Kwahiyo watu wengi walianza kutoka katikakati ya jiji la Dar es Salaam kwa kasi kwa sababu ya woga waliokuwa nao dhidi ya kundi hili.
 Katika baadhi ya maeneo kama Ubungo na Sinza, maduka yalifungwa na biashara nyingine zilisimama kwa kuhofia vijana hawa.

Mimi binafsi nilipata habari hizi kwa kusoma kwenye kurasa za mitandao ya kijamii,  halafu nikapiga simu kwa polisi kuulizia ili nipate habari za uhakika. Polisi walinihakikishia kwamba wanashugulikia suala hilo na kuwa wananchi wasiwe  na wasiwasi .

Baadaye nikapiga simu kwa dada ambaye ni rafiki yangu kuhusu habari hii yeye akasema amesikia vijana hao wametoka mtaa mmoja eneo la Mwananyamala na muda nilioongea nae walikuwa wanaelekea Kinondoni studio .
Kama hii haitoshi niliona baadhi ya picha zilizokuwa zinaonyesha watu wakikimbia. Baadaye niligundua picha hizo ni za tukio la  mlipuko wa mabomu ya Gongo la Mboto miaka kadhaa iliyopita.
Ilibidi niende kwenye ukurasa wa tovuti ya Jeshi la Polisi kuona kama kuna habari hii, hakukuwa na chochote. Pia nilitembelea kurasa ya facebook ya jeshi la polisi sikuona habari yoyote inayohusiana na Panya road. Ilivyokuwa ni kwamba taarifa ya mwisho kwenye ukurasa huo iliwekwa Februari  mwaka 2014.
Sikatai kwamba tukio hilo halikutokea, tukio limetokea lakini jinsi lilivyokuwa linaripotiwa na kutolewa taarifa kuanzia kwa vyombo vyetu vya usalama , wananchi pamoja na vyumba vya habari,  naona kuna haja ya kujipanga vizuri kwenye suala hili ili tusije tukavuruga amani ya nchi yetu huko baadaye.

Tunapenda kuona jeshi la polisi linalokuwa mbele kwenye habari na matukio yanayotokea nchini, kuliko mtu au taasisi nyingine yoyote kwa sababu wao ndio wenye jukumu la kutoa taarifa sahihi na sio mitandao ya kijamii.
Hivi jeshi la polisi linashindwa nini kuwa na jina kwenye kila mtandao wa kijamii kuanzia twitter , facebook , instagram na mengine kwa ajili ya kuhabarisha na pia kutoa ufafanuzi kwa muda muafaka wa jambo au kitu kinapotokea ?
Mimi nilivyopata habari nikapiga simu kwa viongozi wa polisi kisha nikatembelea mtandao wa polisi kwenye mitandao ya kijamii sikuona kitu. Nilitaraji kupata taarifa ya jeshi ili niitumie kuutarifu umma.

Nadhani ni wakati muafaka sasa kwa jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama,  kuwekeza zaidi kwenye mitandao ya kijamii kabla wahalifu na maadui wa nchi yetu hawajaanza kutumia mitandao hii kutuvuruga hasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu .
Tumeona na kusikia jinsi Kenya iliyopitisha sheria fulani ya mawasiliano,  na mwanzoni mwa mwaka huu  kijana mmoja ameshafungwa kwa kumtusi rais wa Kenya.

Hapakwetu  hatujachelewa,  kuna watu wanaandika habari za uongo, kuna watu wanadhalilisha wenzao, kuna watu wanatishia maisha.
Kuna visa vya kunyanyasana na mengine mengi lakini hatuoni wakikamatwa na kuchukuliwa hatua. Matunda ya hali hii ni kama hili la  kusambaza habari za kupotosha na uongo kuhusu Panya road.
Wakati ni huu, hatujachelewa kuwekeza kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi yetu.

No comments:

Post a Comment