Thursday, 22 January 2015

Kura ya maoni

Kwa nini ni vigumu kura ya maoni kufanyika Aprili
*Jaji Warioba aonya mchakato kwenda kinyume na Sheria akibainisha athari zake kuwa ni vurugu katika uchaguzi mkuu.
Wakati Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ukisubiri hatua ya kura ya maoni, wengi wameendelea kutoa maoni yao yanayoonyesha kutofautiana kimtazamo.
Lakini hiyo ndiyo demokrasia ambayo mwisho wa siku hukumu ya kupita au kutopita kwa Katiba Inayopendekezwa itatolewa Aprili 30 mwaka huu kwa kura ya NDIYO na HAPANA.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ni miongoni mwa watu wanaoendelea kutoa maoni yao kuhusu suala hilo. Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya, Jaji Warioba anaonya kuwa maandalizi hayaonyeshi uwezekano wa kura ya maoni kufanyika kwa tarehe iliyopangwa.

Anasema hofu yake ni juu ya kuboreshwa Daftari la wapiga kura sambamba na ratiba ya kura ya maoni, kwa kuwa mwingiliano huo utaleta mkanganyiko.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kasoro zozote zitakazojitokeza kwenye mchakato wa kura za maoni, zitaathiri uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akifafanua Jaji Warioba anasema sheria inaweka utaratibu maalumu wa mchakato wa kura ya maoni ambao inavyoonekana, hautaendana na ratiba ya uboreshwaji wa daftari hilo la kudumu la wapiga kura.
Anasema sheria namba tatu ya mwaka 2014 inayohusu kura ya maoni, inaeleza kuwa jambo la kwanza kufanyika ni uboreshaji wa Daftari la wapigakura na baadaye kufuatiwa na elimu kwa umma kwa miezi miwili, kisha kampeni kwa kipindi cha mwezi mmoja.
“Kwa utaratibu huo uliowekwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itamaliza kazi (kuboresha daftari la kudumu) Machi na wakati huo huo, kura ya maoni imepangwa kufanyika mwezi Aprili,” anasema Jaji Warioba na kuendelea; “Sheria hiyo ya kura ya maoni Na. 3 ya mwaka 2014, inataka wananchi kupewa elimu ya kura ya maoni kwa kipindi cha miezi miwili na mwezi mmoja wa kampeni, lakini hadi sasa hakuna ratiba inayoeleweka.”
“Hii ni Januari, kama watafuata sheria hii na kuanza kutoa elimu kwa kipindi cha miezi miwili, ina maana itakuwa ni Aprili na Mei, ukijumlisha mwezi mmoja wa kampeni ambao ni Juni, ina maana kura itapigwa mwezi Julai. Ikumbukwe kuwa mwezi huo mbio za uchaguzi zitakuwa zimepamba moto,” anasema.
BVR inahitaji kwanza elimu
Jaji Warioba pia akazungumzia matumizi ya BVR katika kura za maoni na uchaguzi mkuu, akisema kwa uzoefu wake, vifaa hivyo vina utata mkubwa, hivyo kunahitajika elimu ya kutosha na umakini mkubwa katika kuvitumia.
“Nilienda Malawi mwaka 2004 na nikaona utaratibu wa BVR umeleta changamoto kwa sababu tu ni teknolojia mpya. Inahitajika elimu ya kina kabla ya matumizi yake,” akaeleza Jaji Warioba.
Akitolea mfano wa utata wa teknolojia hiyo kulingana na uzoefu wake, Jaji Warioba anasema kuwa iwapo mpiga kura atajiandikisha mara mbili au zaidi, mashine hufuta majina yaliyozidi na jina hubaki katika kituo kimoja tu.
Akafafanua kuwa iwapo majina yaliyojirudia yatafutwa ili mpiga kura kujua jina lake lipo katika kituo kipi, ni jambo linalohitaji uhakiki, hivyo baadhi ya watu wataibuka na kudai majina yao hayapo kumbe yamebaki kituo kingine.
Tume ya uchaguzi yanena
Kauli hiyo ya Jaji Warioba inakuja huku kukiwa na taarifa kuwa hadi Januari mwaka huu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilikuwa haijapokea mashine BVR kwa ajili ya kuanza rasmi usajili huo Februari 16 mwaka huu.
Nec imekusudia kupata mashine 8000 ya BVR, lakini hadi Januari 20, ilikuwa bado inasubiri mashine 7750 kutoka kwa kampuni iliyopewa zabuni ya kusambaza vifaa hivyo.
“Bado tunasubiri mashine zisambazwe. Msambazaji bado anafanyia kazi baadhi ya changamoto zilizoonekana wakati wa zoezi la mwanzo la usajili kwa mfumo wa BVR katika majimbo ya Kilombero, Kawe na Mlele,” anasema Mwenyekiti wa Nec, Damian Lubuva.
Uchunguzi wa gazeti hili wakati mashine hizo zikitumika kwa majaribio kwenye majimbo hayo, umebaini kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ikiwamo mashine hizo kupasha joto lililofanya watumiaji wasitishe huduma kwa muda na kusababisha msongamano mkubwa wa watu.
Kuhusu uchaguzi mkuu
Jaji Warioba anasema rais anayetarajiwa kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu anafahamika kwa kuwa katika miaka 50 tangu tupate uhuru, Watanzania wanazijua sifa za kiongozi bora.
“Katika miaka 50 tunazijua sifa za kiongozi bora. Hapa tunakwepa tatizo tu. Tatizo ni matumizi ya fedha na lugha chafu katika kampeni,” alisema Jaji Warioba ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu.
Hadi sasa wanasiasa zaidi ya 20 wakiwamo wa CCM na upinzani wamekuwa ama wanatajwa au wameonyesha nia wenyewe kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Ukiacha wale wanaotajwa, wanasiasa waliotangaza nia hiyo kutoka CCM ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangwala na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed akitangaza nia kupitia ADC.
Akifafanua zaidi, Jaji Warioba anasema kila mtu anaweweseka kuhusu kiongozi anayefaa ingawa ni kazi rahisi kumjua kutokana na ujuzi tulionao wa miaka zaidi ya 50 ya uhuru.
Kadhalika, Jaji Warioba alisema viongozi wa Serikali hawana budi kuangalia taswira ya uchaguzi mkuu ujao kupitia uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao umeonekana kuwa na kasoro zilizosababisha vurugu.
“Nchi hii ina amani na tujitahidi kuilinda amani yetu. Katika uchaguzi huu tufanye kila tuwezalo kuweka maandalizi yenye umakini,” alisema Warioba na kuongeza:  “Nasisitiza  amani. Uchaguzi wa serikali za mitaa ni funzo.”

No comments:

Post a Comment