Maendeleo ya kuridhisha ya Tehama Tanzania
Pamoja na kuwa nchi ya tatu katika ukanda wa Afrika Mashariki katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), jitihada za uwekezaji na matumizi katika teknolojia hiyo, yanatajwa kuipandisha chati Tanzania kimataifa.
Nuzulack Dausen, Mwananchi
Huenda usijue nini kinaendelea wakati unatumia mtandao ofisini kwako au nyumbani kupitia kompyuta, tabiti au simu ya mkononi.
Kasi hiyo ya kuiunganisha nchi kwa mtandao, imeifanya Tanzania kuongeza nafasi yake ulimwenguni katika tasnia hiyo kutoka nafasi ya 127 mwaka 2013 hadi 125 mwaka jana.
Ripoti mpya ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano mwaka 2014 (NRI 2014) iliyotolewa mwishoni mwaka jana, inaonyesha kuwa Tanzania imepanda nafasi mbili kwa kupata alama 3.04 chini ya alama saba zinazotumika kama kigezo cha kupima ubora.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo hutolewa na Taasisi ya World Economic Forums (WEF) kila mwaka, nchi yenye alama 7 ndiyo iliyofanya vizuri zaidi katika nyanja zote za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Nchi 148 zilizofanyiwa utafiti huo katika nyanja za utayari wa kutumia Tehama, upana wa matumizi, matokeo ya teknolojia hiyo kwa jamii na uchumi na namna ubunifu unavyoongezeka na hatua za udhibiti zinazofanywa na Serikali.
Sababu za kufanya vizuri
Utayari wa Serikali katika kukuza Tehama umesaidia kuibeba Tanzania kufikia kiwango hicho baada ya kuwa ya nchi 85 ulimwenguni katika kipimo hicho kidogo cha mwenendo wa ukuaji wa Tehama.
Katika kipengele hicho sheria za kudhibiti Tehama zinaonekana kuimarishwa kuliko miaka ya nyuma kabla ya Sheria ya Posta na Elektroniki ya mwaka 2010 na udhibiti wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Hali kadhalika, matumizi makubwa ya huduma za mtandao serikalini, katika nafasi ya 98 duniani, yaliwezesha mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanakosa huduma hizo huku matumizi ya Tehama katika biashara nayo yakisuasua hadi kuifikisha nchi katika nafasi ya 124 katika kiashiria hicho.
Salamu kwa Serikali
Ujio wa ripoti hiyo mwishoni mwaka jana huenda unatoa salamu kwa Serikali na wadau wengine mwaka huu kuchukua hatua madhubuti ya kukuza sekta hiyo hususan katika matumizi ya mtandao ambayo ripoti imeeleza kuwa ni ghali zaidi na miundombinu yake ni dhaifu.
Kwa viashiria hivyo, ripoti hiyo inaiweka Tanzania katika nafasi ya nne kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya Rwanda iliyoongoza ikiwa nafasi ya 85 ulimwenguni, ikifuatiwa na Kenya (92), Uganda (115) na Burundi inashikilia mkia kwa kuwa nchi ya 147.
“Tanzania inaendelea kuwa nyuma katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kuendeleza miundombinu ya Tehama, kukuza matumizi makubwa ya teknolojia hiyo na pia kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi yanayotokana na shughuli za Tehama,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Licha ya maendeleo ya kusuasua katika kukuza Tehama nchini na baadhi ya nchi za Afrika, WEF inaeleza kuwa nchi hizo zinaendelea taratibu kuwekeza katika miundombinu ya Tehama kwa kuongeza idadi ya watu wanaotumia simu za mkononi na mtandao.
Ripoti imeainisha kuwa mikakati kabambe ya kujenga na kuimarisha miundombinu ya Tehama na kuandaa mfumo rafiki wa ugunduzi na ujasiriamali, ndiyo njia madhubuti zitakazopunguza mwanya uliopo katika dijitali hali kadhalika kuleta mapinduzi katika uchumi na jamii.
Nchi imepiga hatua
Wakati ripoti hiyo ikiainisha hayo, mhadhiri wa Tehama kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Geofrey Karokola anasema ukilinganisha na hali iliyokuwepo miaka minne iliyopita Tanzania imepiga hatua kubwa katika Tehama.
“Tupo pazuri lazima tukubali...tumewekeza sana kwenye miundombinu mbalimbali ya mtandao kama mkonga wa taifa, ‘marine cable’ fibre na sea com ambazo zimepunguza gharama za mawasiliano.
Miundombinu hiyo imesababisha intaneti na upigaji wa simu kuwa rahisi kiasi cha kumfanya kila mtu aweze kunufaika na huduma hizo,” anasema Karokola.
Kwake yeye, Tanzania huenda imefanya vibaya kutokana na ukubwa wa nchi ukilinganisha na Rwanda ambayo ukubwa wake unafanana na mkoa wa Kagera, hivyo ni rahisi kwa nchi hiyo kuonekana bora zaidi katika nyanja hizo.
“Mara nyingi hesabu za watafiti hao hujikita pia kwa kufananisha idadi ya watu na iwapo wanapata huduma za mtandao,’’ anasema na kuongeza:
“Mara nyingine tafiti hizo zinakuwa na tabia ya kuegemea upande mmoja kutokana na baadhi ya viashiria kuachwa. Kwa hali ya kawaida, Tanzania ipo vizuri kuliko Uganda ambayo ipo juu yetu,” anasema mtaalamu huyo aliyefanya tafiti nyingi ya Tehama nchini.
Hata hivyo, anakiri kuwa kuna tatizo kubwa la ubunifu licha ya kuwa na vituo vya kukuza vipaji kama vile Buni na Tanzict na kuongeza kuwa kuna haja ya kuzidi kuwekeza katika eneo hilo.
Kuhusu suala la utaalamu ambalo Tanzania imeshika nafasi ya 129 duniani kati ya nchi 148, Dk Karokola anasema kuna Watanzania wengi wenye taaluma ya Tehama na kwamba kwa sasa karibu kila chuo kikuu au chuo cha kawaida kinatoa mafunzo hayo.
“Hata hivyo, nashauri watumishi wa Serikali na wataalamu wengine wa tasnia hiyo wawe wanapatiwa mafunzo ya kujiongezea utaalamu kila baada ya robo mwaka kwani teknolojia inakua kwa kasi sana,” anaongeza.
No comments:
Post a Comment